Alhamisi 22 Oktoba 2026 - 08:00
Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli Afafanua Kanuni Tatu za Msingi za Maadili ya Kiislamu/ Asisitiza Umuhimu wa Kulinda Mipaka ya Nchi na Kusimama Imara Dhidi ya Uchokozi

Hawza/ Ayatullah Jawadi Amuli amesisitiza umuhimu wa kulinda usalama na heshima ya jamii, pamoja na kuwaunga mkono wapiganaji, akisema: “Mpiganaji anapokuwa katika zamu ya kutekeleza majukumu yake na kulinda eneo analowajibika kulihami, hapaswi kuondoa mkono wake kwenye kifyatulio cha silaha, anapaswa kuwa makini ili asisinzie wala kughafilika.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kila wiki cha darsa ya maadili cha Ayatullah Jawadi Amuli kilifanyika asubuhi ya jana, Jumatano, tarehe 29 Mehr 1405 Hijria Shamsia, katika Msikiti Mkuu wa Qum, kikihudhuriwa na watu wa makundi mbalimbali ya jamii.

Katika kikao hicho, Ayatullah Jawadi Amuli alielezea kanuni kadhaa za maadili ambazo zimepewa msisitizo na Amirul Muuminina Ali (a.s.), huku akifafanua kanuni tatu za msingi ambazo ni uhuru na kujitawala kwa heshima, ghera na uungwana, pamoja na ushujaa katika medani ya vita. Akirejelea hali ya sasa, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia mafundisho hayo, hususan katika kulinda usalama na heshima ya jamii na kuwaunga mkono wapiganaji.

Akieleza kuwa Uislamu una kanuni nyingi za kimaadili, mbali na itikadi na hukumu za kidini, alisema kuwa; baadhi ya kanuni hizo zimepewa uzito mkubwa katika maelezo ya wanazuoni, huku nyingine zikiwa hazijaelezwa kwa kina ipasavyo.

Alisema: “Katika maneno yenye nuru ya Amirul Muuminina Ali (a.s.), kuna baadhi ya kanuni za kimaadili ambazo zimepewa msisitizo wa pekee, miongoni mwa hizo ni uhuru na kujitawala kwa heshima, ghera na uungwana, pamoja na maelekezo yanayohusiana na ushujaa katika medani ya vita.”

Uhuru na kujitawala kwa heshima haviendani na ufisadi, ubadhirifu wa mali na kupandisha bei kiholela

Katika kufafanua kanuni ya uhuru na kujitawala kwa heshima, Ayatullah Jawadi Amuli alirejelea kauli ya hekima ya Amirul Muuminina Ali (a.s.), aliyesema:

«أَلَا حُرٌّ یَدَعُ هَذِهِ اللُّمَاظَةَ لِأَهْلِهَا؟ إِنَّهُ لَیْسَ لِأَنْفُسِکُمْ ثَمَنٌ إِلَّا الْجَنَّةَ، فَلَا تَبِیعُوهَا إِلَّا بِهَا.»

“Je, hakuna mtu huru atakayeacha mabaki haya kwa wenyewe? Hakika, nafsi zenu hazina thamani nyingine isipokuwa Pepo; basi, msiziuze isipokuwa kwa Pepo hiyo.”

Akifafanua maana ya neno lumazah (لماظة), alisema kuwa ni mabaki ya chakula yanayobaki katikati ya meno baada ya kula. Amirul Muuminina Ali (a.s.) anauliza: Je, atapatikana mtu mwenye uhuru wa kweli atakayeacha mabaki hayo kwa wenyewe na asiendelee kuyatafuta?

Ayatullah Jawadi Amuli alihusisha mafundisho hayo na maisha ya kijamii huku akisisitiza kuwa; mwanadamu hapaswi kufuatilia vitu ambavyo vimepitia mikononi mwa wengine na ambavyo wengine tayari wamefaidika navyo, kisha akajenga maisha yake kwa kutegemea mabaki yao.

Alisema: “Imam anauliza: Ni nani aliye na uhuru wa kweli kiasi cha kutokwenda kutafuta chochote katika pipa la taka la kizazi kilichotangulia? Ufisadi huu, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali za umma, pamoja na mambo mengine yanayofanana na hayo, ndilo pipa hilo la taka! Mtu aliye huru kwa maana halisi hapaswi kujiingiza katika mienendo hiyo ili kupata manufaa ya kimali.”

Akizungumzia baadhi ya changamoto za kiuchumi na kijamii, zikiwemo kupandisha bei kiholela, ubadhirifu wa mali na matumizi mabaya ya fedha, alibainisha kuwa: “Uhuru na kujitawala kwa heshima haviendani na ubadhirifu wa mali, ufisadi wala kupandisha bei kiholela. Mwanadamu anapaswa kuendesha maisha yake kwa njia sahihi na kwa juhudi zake mwenyewe, huku akitambua kuwa thamani ya utu wake ni kubwa mno kiasi kwamba hapaswi kujiuza kwa mambo duni na yasiyo sahihi.”

Ayatullah Jawadi Amuli alisisitiza kuwa suala la uhuru na kujitawala kwa heshima ni mlango maalumu katika maadili ya Kiislamu, akakumbusha kuwa, kama vile hukumu za kidini na matendo yanayopendekezwa katika Uislamu kila kimoja kina nafasi yake, vivyo hivyo uhuru na kujitawala kwa heshima ni suala la msingi linalopaswa kufafanuliwa kwa usahihi.

Uzalendo na uungwana ni kulinda heshima ya mipaka na kusimama imara dhidi ya uchokozi

Katika sehemu inayofuata ya mazungumzo yake, Ayatullah Jawadi Amuli alirejelea riwaya zinazohusu uzalendo na uungwana huku akisema kuwa; katika vitabu vya riwaya, kuna msisitizo kuhusu umuhimu wa kulinda mipaka ya heshima na kukabiliana na uvamizi wa kutumia silaha. Hata hivyo, alisema kuwa sehemu hii ya mafundisho ya dini haijapewa uzito wa kutosha ikilinganishwa na baadhi ya mada nyingine.

Akirejelea riwaya kutoka kwa Imam Swadiq (a.s.) na Imam Baqir (a.s.) kuhusu mtu anayeingia katika eneo la mwingine kwa nia ya kushambulia maisha na mali yake, alieleza kuwa riwaya hizo zinasisitiza umuhimu wa kujilinda dhidi ya mshambuliaji. Alinukuu riwaya isemayo:

«اللص يدخل علي في بيتي يريد نفسي ومالي قال اقتله فأشهد اللَّه و من سمع أن دمه في عنقي»

“Mwizi ananiingia nyumbani kwangu akiwa na nia ya kushambulia maisha yangu na kuchukua mali yangu, Imam akasema: Muue, ninashuhudia kws Mwenyezi Mungu na kila aliyesikia hili kuwa damu yake iko juu ya dhamana yangu.”

Pia, imenukuliwa kauli ifuatayo:

«فاقتلوه فما دخل عليك فعلي»

“Basi, muue, kwani chochote atakachokufanyia kwa kuingia kwako kwa nia hiyo, jukumu lake liko juu yangu.”

Ayatullah Jawadi Amuli alifafanua kuwa, ikiwa mtu wa kigeni ataingia nyumbani kwa mtu akiwa na silaha na akikusudia kuidhuru nafsi yake au mali yake, riwaya hizo zinaelekeza katika kumkabili mshambuliaji  alisema kuwa jambo hili linadhihirisha maana ya ghera na uungwana.

Akirejelea riwaya zilizopokewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (a.s.), alibainisha kuwa wajibu wa kujilinda dhidi ya uchokozi na uvamizi umeelezwa kwa uwazi. Kwa hiyo, uzalendo na uungwana ni miongoni mwa mada muhimu katika maadili ya Kiislamu zinazopaswa kuzungumziwa kwa upana zaidi.

Akizungumzia uvamizi wa kijeuri uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran, alisisitiza umuhimu wa kuyazingatia mafundisho hayo katika mazingira ya sasa, hususan katika kulinda mipaka na heshima ya nchi na kusimama imara dhidi ya uchokozi wa wazi wa pande hizo mbili.

Ayatullah Jawadi Amuli alisema kuwa ghera ina maana ya kuondoa nafasi ya mtu mwingine kuingilia eneo lisilomhusu, yaani kutomruhusu mgeni au mtu wa kigeni kuingia katika eneo la heshima la mtu bila haki, pamoja na kukabiliana na uvamizi.

Aliongeza kuwa, kama vile mazungumzo mengi yamefanyika kuhusu Swala, Saumu, Hija na hukumu nyingine za kidini pamoja na matendo yanayopendekezwa, ni muhimu pia mafundisho yanayohusu ghera na uungwana yafafanuliwe zaidi. Hii ni kwa sababu riwaya hizo zinahusu mojawapo ya masuala muhimu ya maisha ya kijamii na wajibu wa mwanadamu katika kulinda heshima na mipaka yake mwenyewe pamoja na ile ya jamii.

Umuhimu wa ushujaa katika medani ya vita na kuwa macho wapiganaji katika kulinda mipaka

Katika mhimili wa tatu wa hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli alizungumzia maelekezo ya Amirul Muuminina Ali (a.s.) kuhusu wapiganaji na umuhimu wa kuwa macho katika medani ya vita. Akirejelea barua ya kumi na moja katika Nahjul Balagha, alisema kuwa sehemu hii ya mafundisho ya Imam Ali (a.s.) inalingana na hali iliyopo kwa sasa.

Akitoa shukrani kwa juhudi na msimamo thabiti wa wapiganaji wanaoshiriki katika medani ya kulinda nchi, alisema: “Wapendwa hawa walioko katika uwanjs vita wanatekeleza majukumu yao katika mazingira ambayo adui anaweza kushambulia wakati wowote. Kwa hiyo, wanapaswa kuwa macho daima, kudumisha utayari wao wa kujilinda na kuweka mikono yao kwenye vifyatulio vya silaha.”

Aliongeza kuwa, “Tunaposema mara nyingi kuhusu watu hawa, ‘Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao’, sababu ni kwamba ni sahaba gani anayeweza kumsaidia Imam wake kwa namna hii?”

Ayatullah Jawadi Amuli alirejelea maelekezo ya Amirul Muuminina Ali (a.s.) kwa wapiganaji katika barua ya kumi na moja ya Nahjul Balagha, akainukuu kauli ifuatayo:

«وَ لَا تَذُوقُوا النَّوْمَ إِلَّا غِرَاراً أَوْ مَضْمَضَةً»

“Wala msionje usingizi isipokuwa kwa muda mfupi sana.”

Alieleza kuwa Imam Ali (a.s.) anawanasihi wapiganaji wasilale isipokuwa kwa muda mfupi unaohitajika tu. Kama vile mtu aliyefunga anavyoweza kuweka maji kinywani mwake na kuyazungusha bila kuyameza, ndivyo mpiganaji anavyopaswa kujiepusha na usingizi wa kughafilika anapokuwa katika zamu ya ulinzi na kulinda eneo alilokabidhiwa, anapaswa kudumisha umakini na kuwa macho wakati wote.

Akisisitiza kuwa maelekezo haya yanahusu mazingira ya ulinzi na wajibu wa wapiganaji katika medani ya kujilinda, alisema kuwa; mwanadamu hawezi kupita usiku na mchana bila kupumzika, na kwamba uchovu ni jambo la kawaida. Hata hivyo, mpiganaji anapokuwa katika zamu ya kutekeleza majukumu yake na kulinda eneo analowajibika kulihami, hapaswi kuondoa mkono wake kwenye kifyatulio cha silaha, anapaswa kuwa macho ili asishindwe na usingizi wala kughafilika. Katika mazingira kama hayo, alieleza kuwa mapumziko yanapaswa kupangwa kwa namna ambayo haitasababisha kupoteza utayari na umakini unaohitajika katika kutekeleza wajibu wa kujilinda.

Kuiga mfano wa Nabii Ibrahim (a.s.): Kupambana na ibada ya sanamu na kusimama imara dhidi ya adui

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli alirejelea aya tukufu ya Qur’ani inayosema:

«وَاتَّبِعُوا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ»

“Na fuateni dini ya Ibrahim.”

Alisisitiza umuhimu wa kuiga mwenendo wa Nabii Ibrahim (a.s.). Akizungumzia mapambano ya Nabii Ibrahim (a.s.) dhidi ya ibada ya sanamu na kitendo chake cha kuvunja sanamu, alisema kuwa Qur’ani Tukufu inawataka wafuasi wa Uislamu kufuata dini ya Nabii Ibrahim (a.s.).

Alieleza: “Anawaambia kwamba, kwa kuwa ninyi mmeukubali Uislamu, mmezaliwa katika mazingira ya Uislamu na ni watoto wa watu wenye hadhi, basi ninyi ni miongoni mwa kizazi cha Khalilur-Rahman Ibrahim na watoto wake. Kama vile Ibrahim Khalil alisimama imara dhidi ya ibada ya sanamu na akapambana na sanamu kwa kutumia shoka, ninyi pia mnapaswa kuchukua shoka na kuwa wavunjaji wa sanamu.”

Ayatullah Jawadi Amuli alihusisha mafundisho hayo na hali ya sasa, akisema kuwa Nabii Ibrahim (a.s.) alipambana na sanamu kwa kutumia shoka, na kwamba leo hii, kulingana na mazingira yaliyopo, inapaswa kutumia zana na vifaa vinavyohitajika, kama vile makombora, katika kukabiliana na adui.

Alisisitiza kuwa, kama vile Nabii Ibrahim (a.s.) alivyopinga ibada ya sanamu na kusimama imara dhidi yake, vivyo hivyo wafuasi wake wanapaswa kuwa na msimamo thabiti na uvumilivu katika kulinda dini yao, heshima yao na uhuru wao wa kujitawala.

Mwisho wa hotuba yake, Ayatullah Jawadi Amuli alisoma dua kwa ajili ya wananchi wa Iran, wapiganaji, wanazuoni na watumishi wote wa jamii. Alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajalie wote manufaa na neema na uangalizi wa Ahlul-Bayt (a.s.), na awape wananchi wa Iran heshima, utu, utukufu na mafanikio katika maisha ya dunia na Akhera.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha